CHUO KIKUU MZUMBE WAANZA KUTOA HUDUMA MAONESHO YA SABASABA

 
Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yameanza kushika kasi ikiwa ni siku ya pili huku wananchi wa jiji la Dar es Salaam wakimiminika kupata huduma na kujionea bunifu za kiteknolojia na ujasiriamali zinazofanywa na wanafunzi chini ya usimamizi wa wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe ikiwa ni miongoni mwa washiriki kwenye maonesho hayo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari waliofika katika banda la Chuo Kikuu Mzumbe lililopo karibu na Jukwaa kuu, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Chuo hicho Bi. Lulu Mussa amewakaribisha Wananchi wote kutembelea maonyesho hayo na hasa katika banda la Mzumbe kujionea shughuli zinazotekelezwa na chuo hicho kikubwa cha umma nchini.
“Tupo hapa kuwahudumia wateja wote na tunafanya usajili wa papo kwa hapo kwa Wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo kwa fani mbalimbali katika mwaka wa masomo 2024/2025, usajili huu unahusisha ngazi zote kuanzia Astashahada, Stashahada, Shahada za Awali na Shahada za Umahiri” Alisisitiza Bi. Mussa
Aidha amesema kuwa mbali na udahili, Chuo Kikuu Mzumbe pia kinatoa ushauri wa kisheria bure kwa wananchi wote watakaofika kutembelea maonesho hayo kwa kipindi chote cha maonesho, pamoja na kuonesha wananchi shughuli mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi na wahadhiri kupitia bunifu mbalimbali kama vile mifumo ya Sayansi na teknolojia inayolenga kutatua changamoto katika jamii, pamoja na ujasiriamali. Maeneo mengine ni shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo kupitia miradi ya ufadhili iliyolenga kuihudumia Jamii.
Chuo Kikuu Mzumbe kinashiriki kwa mara nyingine maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 48 yaliyoanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu katika viwanja vya kimataifa vya Mwl.Julius Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jiji Dar es Salaam kikijivunia kuwaonesha Wananchi na wadau wa elimu utekelezaji wa majukumu yake makuu ambayo ni kutoa mafunzo, kufanya tafiti, kutoa shauri elekezi na huduma kwa jamii.

Address

Mzumbe University,
Dar es Salaam Campus College,
Upanga Area Plot No. 941/2 Olympio Street,
P.O.Box 20266, Dar es Salaam, Tanzania
General Line: +255 (0) 22 2152582,
Direct Line: +255 (0) 22 2152586,
Fax: +255 (0) 22 2152584/2150398,
Cell: +255 (0) 689 455 588,
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. || This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

About us

Social Connect