RASI WA CHUO KIKUU MZUMBE NDAKI YA DAR ES SALAAM AWAHIMIZA WANACHUO KUTUMIA TEKNOLOJIA KUKUZA TAALUMA

RASI wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es salaam Prof. Cyriacus Binamungu amewahimiza wanachuo wa Ndaki hiyo kutumia Teknolojia zilizopo ikiwemo TEHAMA na mifumo mingine ya maktaba ili iwasaidie katika masomo yao.
 
Prof. Binamungu ametoa rai hiyo Aprili 16, 2024 wakati akizungumza na wanafunzi wa Shahada ya Awali Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wanaosoma kituo cha Tegeta ikiwa ni sehemu ya kuwakumbusha wajibu wao.
"Katika ulimwengu tunaokwenda wa sasa hamuwezi kukwepa matumizi ya TEHAMA kwani inaongeza na kupanua uelewa katika yale mnayojifunza iwapo hamtaitumia vibaya." Alisitiza Prof. Binamungu.
 
Aidha, Rasi huyo wa Ndaki amewakumbusha wanafunzi kuhusu umuhimu wa kujiheshimu kwa kuthamini utu wao na kushiriki michezo ambapo pia ameweza kuchangia ununuzi wa mipira miwili kwa timu ya mpira wa miguu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Shahada za Awali kituo cha Tegeta, ambaye pia ni Mratibu wa Dawati la Jinsia Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Janeth Swai, amewasisitiza wanafunzi kutoa taarifa za changamoto zozote wanazokumbana nazo ili ziweze kutatuliwa na zisiwe kikwazo katika masomo yao.
" Dawati la Jinsia ni kwa wote kwa maana ya wanawake na wanaume, mnapokutana na changamoto msikae nazo, mje tuweze kuongea na kuweza kuzitafutia ufumbuzi." Alieleza Dkt. Swai.
 
Mshauri wa Huduma za Wanafunzi Bi. Zitta Victoria Mnyanyi amewataka wanafunzi hao kuzingatia maelekezo waliyopewa ili waweze kutimiza malengo yao wawapo chuoni.
Akishukuru kwa niaba ya wanafunzi wenzake Bw. Edgar Missingo Mwanafunzi wa Shahada ya Utawala wa Umma mwaka wa tatu aliushukuru uongozi wa Ndaki kwa kuwakumbusha wajibu wao kama wanafunzi wawapo chuoni licha ya kuwa viongozi pia wamekuwa wakibeba jukumu la wazazi la kuwakumbusha masuala ya kitaaluma na kijamii.
Kikao hicho kilishirikisha wanafunzi wote wa Shahada ya Awali mwaka wa kwanza hadi wa tatu ambao wanasoma Shahada.
 
*********************
 

 

Address

Mzumbe University,
Dar es Salaam Campus College,
Upanga Area Plot No. 941/2 Olympio Street,
P.O.Box 20266, Dar es Salaam, Tanzania
General Line: +255 (0) 22 2152582,
Direct Line: +255 (0) 22 2152586,
Fax: +255 (0) 22 2152584/2150398,
Cell: +255 (0) 689 455 588,
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. || This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

About us

Social Connect