RC MTAKA AAHIDI MKOA WAKE KUWA WA KWANZA KUTUMIA MFUMO WA AFYA ULIOBUNIWA NA MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU MZUMBE

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka, ametembelea Banda la Chuo Kikuu Mzumbe na kuvutiwa na bunifu za wanafunzi wa Chuo hicho, walioshiriki kwa mara ya kwanza kwenye maonesho ya Ubunifu, Sayansi na Teknolojia “MAKISATU” chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Mhe. Mtaka, amevutiwa na ubunifu wa mfumo wa Afya, ambao umelenga kupunguza vifo vya akina mama na Watoto, kwa kuweka mfumo rahisi wa mawasiliano kati ya mama na kituo cha afya, wakati wote wa ujauzito hadi kujifungua.

Aidha, ameahidi mkoa wake kuwa wa kwanza kutumia mfumo huo, kwa kuanza kuufanyia majaribio kwa kuhusisha wataalamu wa afya, ili mafanikio ya mfumo huo kuanza kuonekana kwa wananchi.

“Ni muhimu bunifu hizi zilizolenga kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii zikaendelezwa na kuleta matarajio yaliyokusudiwa kwa mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti, na mimi naahidi kuwa wa kwanza kuanza kutumia mfumo huu na nitamwagiza Mganga Mkuu wa mkoa wa Dodoma, kufika katika Banda la Chuo Kikuu Mzumbe, kujionea ubunifu huu wa kufuatilia afya ya mama Mjamzito na tuanze majaribio mara moja” alisema

Mfumo wa kufuatilia maendeleo ya afya ya mama Mjamzito, umebuniwa na Mwanafunzi Adelina Deusdedith, wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia cha Chuo Kikuu Mzumbe.

Mifumo mingine iliyobuniwa ni pamoja na mfumo wa kudhibiti bidhaa bandia, ugunduzi wa gesi ya kupikia inayozalishwa kwa kinyesi, pamoja na ufugaji wa nzi, ambao wanazalisha chakula cha mifugo ikiwemo Samaki.

Chuo Kikuu Mzumbe kimeshiriki kwa mara ya kwanza maonesho ya Kitaifa ya Ubunifu (MAKISATU) yaliyozinduliwa jijini Dodoma Mei 16, na kufungwa rasmi leo Mei 19 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango.

*************************************************************************************************************

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Antony Mtaka (kushoto) akizungumza na baadhi ya Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe ambao ni Mkuu wa Kitivo cha Sayansi za Jamii, Dkt.Harold Uttoh (wa pili kushoto) ,Meneja wa Ubunifu,Ujasiriamali na Ushirikiano wa Kibiashara Dkt.Nicholaus Tutuba na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Masoko Bi.Rose Joseph.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Antony Mtaka akisaini kitabu cha Wageni katika banda la Chuo Kikuu Mzumbe, anayeshuhudia kulia ni Inj.Dkt.Mourice Daud, Mhadhiri na Mlezi wa Wanafunzi wa bunifu wa mifumo ya kiteknolojia

 

 

Address

Mzumbe University,
Dar es Salaam Campus College,
Upanga Area Plot No. 941/2 Olympio Street,
P.O.Box 20266, Dar es Salaam, Tanzania
General Line: +255 (0) 22 2152582,
Direct Line: +255 (0) 22 2152586,
Fax: +255 (0) 22 2152584/2150398,
Cell: +255 (0) 689 455 588,
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it..

About us

Social Connect