MZUMBE YAELEZA SIKU 365 ZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN NA DHAMIRA YA DHATI YA MAGEUZI KATIKA SEKTA YA ELIMU

Chuo Kikuu Mzumbe ni Chuo Kikuu cha Umma nchini ambacho kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Chuo Kikuu Mzumbe Na. 21 ya mwaka 2001. Sheria hiyo ilifutwa na Sheria ya Vyuo Vikuu Na. 7 ya mwaka 2005 ambayo ni sheria inayosimamia masuala yote yanayohusu Elimu ya Chuo Kikuu nchini Tanzania. Kwa sasa, Chuo kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Hati Idhini ya Chuo Kikuu Mzumbe, 2007 iliyotolewa chini ya Kifungu Na. 25 cha Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005.

Historia ya Chuo Kikuu Mzumbe ilianza kabla ya Uhuru wa Tanganyika ambapo mwaka 1953 Serikali ya Kikoloni ya Uingereza ilianzisha Kituo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa machifu, maakida na watumishi wengine katika Serikali za Mitaa za wakati huo. Kituo hicho kilianzishwa katika eneo la Mzumbe lililoko Wilaya ya Mvomevo katika Mkoa wa Morogoro ambapo ndio Makao Makuu ya Chuo yalipo sasa. Baada ya Uhuru, Serikali iliendelea kupanua miundombinu na aina ya programu zilizokuwa zinazofundishwa katika Kituo hicho na mwaka 1963 kiliunganishwa na Kituo cha Mafunzo ya Mendeleo Vijijini Tengeru na kuitwa Kituo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini Mzumbe na kupanua uwigo wa fani za mbalimbali hususani katika maeneo ya utawala na menejimenti, sheria, ushirika, n.k. Mwaka 1972, Serikali ilikipandisha hadhi Kituo hicho na kuwa Chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe (“Institute of Development Management Mzumbe, IDM Mzumbe”) kwa kuunganisha Taasisi ya Utawala wa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kituo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini Mzumbe. Chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe kilipewa jukumu la kutayarisha watendaji katika Taasisi za Umma. Kutokana na kukua kwa kwasi kwa IDM Mzumbe na kuongezeka kwa mahitaji ya viongozi wa kusimamia uendeshaji wa Taasisi za Umma, Serikali iliamua kukipandisha hadhi na kuwa Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 2001. Chuo kimeendelea kukua kwa kasi kwa idadi ya wanafunzi na wafanyakazi na na kwa sasa, kina matawi tatu, yaani, Kampasi Kuu liyopo Morogoro, Ndaki ya Dar es Salaam na Ndaki ya Mbeya.

Majukumu makubwa ya Chuo ni kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kufanya utafiti, kutoa ushauri wa kitaalam na huduma kwa jamii. Kwa sasa, Chuo Kikuu Mzumbe kinaendesha programu 77 za masomo katika maeneo yaliyoianishwa hapo juu katika ngazi za Astashahada (9), Stashahada (7), Shahada za Kwanza (29), Shahada za Umahiri (32) na Shahada za Uzamivu (“PhD”). Chuo kinatoa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fan izote zilizoainishwa hapo juu. Maeneo ambayo Chuo Kikuu Mzumbe kina kimejijengea umahiri na ubobevu kwa miaka mingi ni pamoja na Utawala wa Umma; Menejimenti ya Rasilimali Watu, Serikali za Mitaa, Mifumo ya Afya na Mazingira; Ufuatiliaji na Tathmini Katika Afya; Uongozi wa Biashara, Ujasiriamali na Ubunifu; Uhasibu na Fedha, Ununuzi na Ugavi; Uchumi ikiwa ni pamoja na Mipango na Sera, Mipango na Menejimenti ya Miradi na Maendeleo ya Watu); Sheria; Elimu (Hisabati na Lugha; Biashara na Uhasibu); Teknolojia ya Habari (Menejimenti ya Mifumo; Menejimenti ya Habari); Sera za Umma; Sayansi ya Menejimenti ya Uhandisi wa Viwanda na Menejimenti ya Uzalishaji na Usimamizi pamoja  na maeneo mengine kama yanavyopatikana kwenye tovuti ya Chuo Kikuu Mzumbe (www.mzumbe.ac.tz).

Kati ya viongozi wengi walioshika nyadhifa nyeti katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliosoma IDM-Mzumbe ni pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Jumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe inayo kila sababu ya kufurahia mafanikio ya Mhe. Samia Suluhu Hassan katika mwaka wake wa kwanza kama Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwani kwa umahiri katika uongozi ambao ameuonesha kama Rais na pia, uzalendo ambao unajidhihirisha katika uongozi wake ni uthibitisho wa kutosha kudhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa wahitimu bora wa Utawala wa Umma waliosoma katika Chuo hiki.

Mafanikio Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan

Chuo Kikuu Mzumbe ni mojawapo ya Taasisi za Elimu ya Juu ambazo zimenufaika sana katika kipindi chote ambacho Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa Kiongozi wa Ngazi ya Juu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia akiwa Makamu Makamu wa Rais katika Serikali ya Awamu ya Tano na sasa, kama Rais wa Awamu ya Awamu ya Sita.

Katika kipindi cha uongozi wake, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu nchini hususani katika katika uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga miundombinu mipya na kuboresha miundombinu iliyopo. Miundombinu iliyojengwa  na kuboreshwa ni pamoja na ifuatayo:

  • Kukamilika ujenzi na uwekaji wa samani katika mabweni manne (4) ya wanafunzi katika Kampasi Kuu ya Chuo ambayo ujenzi wake ulikamilika mwaka 2021. Uwekaji wa samani vikiwemo vitanda, meza, makabati, magodoro, viti mwezi Februari 2022 na kwasasa ujenzi wa Kantini unaendelea ili kuruhusu majengo hayo kuanza kutumika. Ujenzi wa hosteli hii umegharimu takribani shilingi bilioni 7.7. Mabweni haya yataanza kutumika kwa malazi ya wanafunzi 1,024 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kantini ya chakula ambao unaendelea. Kuanza kutumika mabweni haya kutaongeza nafasi za malazi ya wanafunzi katika Kampasi Kuu ya Chuo, kutoka 2,718 zilizopo sasa hadi 3,742, na hivyo, kupunguza kwa kiasi kikuwa tatizo la uhaba wa nafasi za malazi chuoni.
  • Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la taaluma lenye kumbi za mihadhara mbili (2) na madarasa manne (4) ambayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja pamoja na ofisi kwa ajili ya wafanyakazi 50 katika Kampasi Kuu ya Chuo. Ujenzi wa jengo hilo pamoja na kuweka samani umegharimu takribani TShs. Bil 3.1.
  • Kukamilika kwa ujenzi jengo la utawala na madarasa katika Ndaki ya Mbeya lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 908 kwa wakati mmoja na ofisi kwa ajili ya wafanyakazi 48. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu takribani TShs. Bil. 3.1.
  • Kukamilika kwa ukarabati wa majengo na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa ajili ya kuanzisha masomo ya Shahada za Kwanza katika Kituo cha Tegeta, Ndaki ya Dar es Salaam. Ukarabati huo ambao ulihusisha madarasa tisa (9) kumbi za mihadhara mbili (2) maabara ya kompyuta na maktaba umegharimu takribani shilingi 1.3 bilioni. Kwa sasa, jumla ya wanafunzi 414 wamesajiliwa kusoma Shahada za Kwanza katika Utawala wa Umma, na Uhasibu na Fedha katika Kituo hicho.

Uwekezaji katika kujenga na kuboresha miundombinu umekiwezesha Chuo Kikuu Mzumbe kuongeza idadi ya wanafunzi 11,967 waliosajiliwa katika mwaka wa masomo wa mwaka 2019 hadi wanafunzi 13,074 mwaka wa masomo wa 2021/22. Vilevile chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Chuo kimenufaika sana kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaopata Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Idadi ya wanafunzi wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu, imeendelea kuongezeka kutoka 3,701 mwaka 2019 hadi 5,109 mwaka 2022, ambapo kiasi cha zaidi ya TShs. Bil 18.1 kilitolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini kulipia gharama za malazi, chakula, masomo n.k Ongezeko hilo linafanya jumla ya wanafunzi waliokidhi vigezo na kunufaika na mikopo ya Elimu ya Juu kati mwaka 2019 hadi 2022 kufikia 13,027,  miongoni mwao wanawake wakiwa 5,415 (sawa na 42%)  na Wanaume 7,612 (sawa na 58% ). Kwa mwaka wa masomo 2021/22 peke yake, jumla ya kiasi cha shilingi 3.5 bilioni zimetolewa kwa ajili ya wanufaika 5,109 (wanaume 2,924 na wanawake 2185). Kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wa mkopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kumechochea vijana wengi kujiunga na Elimu ya Juu ikiwa ni pamoja na wale wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini na hivyo, Taifa letu limepiga hatua kubwa katika kuzalisha wataalam wa ngazi mbalimbali wenye ujuzi na maarifa kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi yetu.

Kwa sasa, Chuo kimo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (‘Higher Education for Economic Transformation, HEET) ambao unatekelezwa na Vyuo Vikuu vya Umma chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia. Katika Mradi huu, Chuo Kikuu Mzumbe kimetengewa takribani Dola za Kimarekani milioni 21 (takribani TShs. bilioni 50). Katika Mradi huu, Chuo kinategemea kutekeleza miradi 10 ya ujenzi wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na kumbi za mihadhara, madarasa, maktaba, miundombinu ya TEHAMA, ofisi za wafanyakazi, atamizi ya ubunifu na biashara, miundombinu ya maji safi na majitaka na miundombinu mingine wezeshi. Miundombinu itakayojengwa inategemewa kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 13,074 waliopo sasa hadi takribani wanafunzi 17 ,000 mwaka 2026/27. Miradi hii tayari imeingizwa katika Mpango Mkakati wa Tano wa Chuo Kikuu Mzumbe (2021/22 – 2025/26) na Mpango Mkuu wa Chuo (2021/22 – 2045/46).

Zaidi ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi katika Chuo Kikuu Mzumbe, Mradi wa HEET unategemewa kuleta mageuzi makubwa katika aina ya wahitimu wanaotoka chuoni kwani Mradi utawezesha kutayarisha mitaala ambayo mkazo wake ni mafunzo wa vitendo zaidi na kufanya kazi kwa karibu na viwanda au Sekta Binafsi ili wahitimu wawe na uwezo wa kujiajiri na kutengeneza ajira au biashara badala ya kutegemea kuajiriwa baada ya kuhitimu. Hii ni katika kutekeleza matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa (2021/22 – 2025/26) ambazo zimeweka mkazo katika sayansi, teknolojia na ubunifu kwa ajili ya kukuza ajira na uchumi wa Tanzania, Vyuo Vikuu vikiwa ni washiriki muhimu katika kutimia azma hii.

Maendeleo makubwa katika Chuo Kikuu Mzumbe ambayo yamepatikana ndani ya muda mfupi ambapo Mhe. Samia Suluhu Hassani amekuwa madarakani ni uthibitisho mwingine wa kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu na kwa umahiri mkubwa. Uongozi wake mahiri umeleta heshima kubwa kwa nchi yetu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, Afrika na duniani kote. Hii imejidhirisha zaidi kwenye Diplomasia ya Uchumi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa wawekezaji katika Sekta mbalimbali nchini kwetu.

Tunampongea sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza mwaka mmoja akiwa madarakani kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo ameonesha umahiri wa hali ya juu katika kuongoza Watanzania na kusimamia rasilimali za nchi yetu kwa manufaa ya wananchi wetu. Tunamwombea mafanikio zaidi katika kuongoza Taifa letu ili kuleta maendeleo na mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi. Sisi wana Jumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe tutaendelea kumuunga mkono kwa kutekeleza Kauli Mbiu ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Kazi Iendelee” kwa kueendeleza kazi ambayo Watanzania wametudhamini kuifanya tukisimamia Kauli Mbiu ya Chuo inayosema “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”.

   ****************************************************************************************************

Mabweni manne (4) ya wanafunzi katika Kampasi Kuu ya Morogoro ambayo ujenzi wake ulikamilika mwaka 2021,

Ujenzi wa hosteli hii umegharimu takribani shilingi bilioni 7.7  na yataanza kutumika kwa malazi ya wanafunzi 1,024

mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kantini ya chakula ambao unaendelea.

 

Jengo la taaluma lenye kumbi za mihadhara mbili (2) na madarasa manne (4) ambayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi

1,000 kwa wakati mmoja pamoja na ofisi kwa ajili ya wafanyakazi 50 katika Kampasi Kuu ya Chuo. Ujenzi wa jengo hilo

pamoja na kuweka samani umegharimu takribani TShs. Bil 3.1

Jengo la utawala na madarasa katika Ndaki ya Mbeya lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 908 kwa wakati mmoja na ofisi kwa ajili ya wafanyakazi 48. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu takribani TShs. Bil. 3.1

 

 

Address

Mzumbe University,
Dar es Salaam Campus College,
Upanga Area Plot No. 941/2 Olympio Street,
P.O.Box 20266, Dar es Salaam, Tanzania
General Line: +255 (0) 22 2152582,
Direct Line: +255 (0) 22 2152586,
Fax: +255 (0) 22 2152584/2150398,
Cell: +255 (0) 689 455 588,
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it..

About us

Social Connect